Polisi watadhibiti mechi za mpira na sherehe za harusi Kwale

Na Sakina Chiro

Idara ya usalama katika kaunti ya Kwale imetangaza hatua za kudhibiti sherehe za harusi kutokana na ongezeko la visa vya utovu wa usalama kaunti hio. 

Idara hio pia imesema kuwa inanuia kudhibiti mechi za mipira.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kauntiya Kwale Ali Nuno, makundi ya kihalifu yamekuwa yakitumia mechi za mpira na harusi kuzua vurugu na kukata watu mapanga.

Nuno amesema hilo limekua likihujumu usalama wa wakaazi.

“Kwanzia Sasa hatutaruhusu sherehe za harusi na mpira kufanyika bila taarifa kutoka kwa polisi,” Nuno alisema.

Akizungumza katika kituo cha polisi cha Diani wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuimarisha usalama almaarufu panga boys campaign, Nuno alisema ni jambo la kusikitisha kuona watoto wadogo wakitembea na mapanga na kudhuru watu hadi kwa maharusi bila wazazi kutilia maanani athari zake.

“Ni aibu gani wazazi nawauliza,kwa nini mruhusu watoto wacheze na mapanga kwenye harusi? Panga ni ya nini na mko kwa sherehe?” Nuno aliuliza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa wadi ya Kinondo Juma Maone aliahidi kushirikiana na polisi kutatua visa vya utovu wa usalama.

Mwenzake wa Bongwe Gombato Tumaini Mwachaunga, aliwaonya wazazi kutohusisha wanasiasa punde watoto wao watakaposhikwa na visa vya uhalifu.

Katika kampeni hiyo,pikipiki nne zilizinduliwa ili kusaidia polisi kupiga doria.

Maeneo ya Markaz, Mwamambi, Tiwi, Ng’ombeni, Mwabungo na Mbuwani yalitajwa kuwa yalioathirika zaidi kwa utovu wa usalama.

Scroll to Top