Wamiliki wa nyumba za bei nafuu Pwani wataanza kupokezwa funguo Disemba mwaka huu

Na Jumwa Mwandoro

Serikali kuu kupitia idara ya ujenzi wa nyumba na maendeleo ya miji itaanza kuwapokeza funguo wamiliki wa nyumba za bei nafuu eneo la Pwani kwanzia tarehe 10 Disemba mwaka huu.

Kulingana na mkurugenzi wa idara hiyo ukanda wa Pwani na Kaskazini Mashariki John Karanja, mradi wa ujenzi wa nyumba hizo huchukua takariban miezi 18 katika maeneo tofauti inakotekelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kwale Karanja alisema kwa jumla kaunti ya Kwale itafaidi na zaidi ya nyumba elfu 10.

“Mradi huu unalenga kufaidi mwananchi wa kiwango chochote cha mapato, pia utafungua ajira hususan kwa vijana na sekta ya juakali,” Karanja alisema.

Karanja amesema kwamba ujenzi wa nyumba za Matuga zilizoko Kwale mjini umefikia  asilimia 13 huku nyumba 192 zikitarajiwa kujengwa Kwa gharama ya shilingi milioni 550.

Miradi sawia itatekelezwa katika eneo la Mabokoni na Diani White House na Survey Camp mjini Kwale,

 “Tumebaini sehemu ya Whitehouse ina mapango hivyo tunataka kuhusisha wenzetu wa makavazi ya kitaifa kuifanya sehemu hiyo kama kivutio cha utalii ili kuongeza thamini mradi wetu na kuzidisha mapato kwa taifa,” Karanja aliongeza.

Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi wa Nyumba na Maendeleo ya Miji Pwani na Kaskazini Mashariki John Karanja akihutubia waandishi wa habari mjini Kwale

Nae waziri ardhi wa serikali ya kaunti ya Kwale Saumu Beja amesema mazungumzo ya jinsi kipande hicho cha ardhi ya serikali cha White House kitakavyotumika bado yanaendelea huku akieleza kuwa serikali tayari imetenga sehemu zengine za kufanikisha mradi huo.

Saumu ameeleza kuwa serikali Iko tayari kupokea mradi wowote utakao mfaidi mkaazi sawia na kuleta maendeleo kwa Jamii.

“Tumepeana takribani hekari 50 za ardhi katika wadi tofauti tofauti ili kutekeleza mradi wa nyumba za bei nafuu lakini hatukuweza kuafikiana na wakaazi baada yao kuwasilisha kesi mahakamani pia sehemu kuwa ndogo na baada ya mkandarasi kuzuru sehemu hiyo alibaini mapango hivyo kuisihi serikali kuwatafutia sehemu mbadala,” Saumu alieleza.

.

Scroll to Top