Uhuru wa vyombo vya habari na mashirika ya kijamii bado wayumba  

Na Caroline Katana

Uhuru wa vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za kibnadamu uko hatarini kote duniani.

Haya ni kwa mujibu wa balozi wa Jumuiya ya umoja wa Ulaya (EU) nchini Kenya Henriette Geiger.

Geiger amesema mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari  na usambazaji wa habari za uongo yangali yanashuhudiwa kote ulimwenguni licha ya hatua zilizopigwa kukabili.

Balozi huyo alikua akizungumza katika katika kongamano la pili la kila mwaka la waandishi  wa habari na mashirika ya kijamii katika eneo la Westlands jijini Nairobi.

Kongamano hilo liliandaliwa na muungano wa waandishi habari nchini kenya (KCA) na shirika la  Civil Freedom Forum  (CFF) kwa ushirikiano na mashirika mengine likiwemo Pen Kenya, Article 19  na Haki Yetu.  .

Kauli mbiu ya kongamano hilo ikiwa ni “Kuimarisha ushirikiano wa mashirika ya kijamii na vyombo vya habari katika ulinzi wa nafasi  ya kiraia“

Balozi Geiger alisema waandishi wa habari katika jamii wana mchango mkubwa wa nikuhabarisha na kuelimisha umma.

Aidha alidokeza kuwa mabadiliko katika tasnia hii yanazua changamoto haswa katika utendaji na uwajibikaji wa wanahabari.

”Uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mashirika ya kijamii ni muhimu katika kila taifa duniani, yanakuza haki za kidemokrasia ila inahuzunisha kuona uhuru wa sekta hizo mbili ukikiukwa kote ulimwenguni” alisema balozi Geiger.

Balozi wa EU nchini Kenya Henriette Geiger

Balozi huyo pia alisema kuwa licha ya wanahabari na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya kukabiliwa na changamoto za uhuru, Kenya imejizatiti katika kutoa nafasi kwa waandishi wa habari na wanaharakati kutekeleza wajibu wao ikilinganishwa na mataifa mengine duniani.

“Mnaeza dhania kuwa mambo nchini Kenya sio mazuri lakini nataka kuwambia kuwa hapa Kenya mambo ni mazuri ikilinganishwa na jinsi hali inavyoshuhudiwa katika mataifa mengine” aliongeza.

Hata hivyo Geiger  ameeleza  kuwa  awali  vyombo vya habari  na mashirika ya kijamii yalikuwa dhabiti katika maswala ya kutetea haki kwa kupaza sauti za wakenya  na kufuatilia maswala mbali mbali  yanayohusiana na taifa hili kinyume na ilivyo sasa  .

“Kusingekuwapo na vyombo vya habari ,wakenya hawangefahamu mambo muhimu yanayoendelea humu nchini na ulimwengu kwa ujumla, ninafahamu kuwepo na kesi za ukiukaji wa haki za  wanahabari na wanaharakati nchini Kenya ,na huu ni mtindo unaoshuhudiwa kote ulimwenguni,” Geiger alisema.

Kadhalka amedokeza kuwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya  inapania kuanzisha mpango  wa kuwajenga uwezo waandishi wa habari wa kitengo cha uchunguzi nchini Kenya ili kuhakikisha kuwa haki zao hazikiukwi  wanapotekeleza majukumu yao .

Kutokana na uwajibikaji wa vyombo vya habari na mashirika ya utetezi  nchini  Kenya balozi Geiger ameelezea umuhimu wa kuondolewa kwa sheria zinazowakandamiza waandishi habari na mashirika ya watetezi ili kuwajengea mazingira salama ya kikazi  .

“Kama Jumuiya ya umoja wa ulaya tunaunga mkono maswala ya utetezi wa haki za kibinadam na mashirika ya kijamii  duniani  kupitia bajeti maalum ambapo zaidi ya asilimia 60 imetengwa kushughulikia maswala mbalimbali kila mwaka ,”Adokeza balozi Geiger.

Akigusia swala la utumizi wa akili bandia maarufu Artificial Inteligence (AI), Geiger amewataka waaandishi wa habari kuchukua tahadhari dhidi ya utumizi wa kifaa hicho katika uchambuzi wa habari.

“Ulimwengu unabadilika kwa haraka sana kupitia utandawazi ,ni sharti waandishi habari wawe makini na kutambua uzuri na madhara yanayotokana na teknologia za kisasa ,kuunganishwa kwa akili bandia katika uandishi wa habari nchini Kenya kama ilivyo katika sehemu nyengine duniani, umeleta fursa na hatari,”alisema balozi huyo. .

Jumuiya ya umoja wa Ulaya  ikishikilia kwamba itaendelea kupigania uhuru wa vvyombo vya habari na mashirika ya kijamii ,huku akitoa wito kwa wakenya kuheshimu nguvu za wengi, akisema kuwa nguvu za wengi ni muhimu katika utatuzi wa changamoto msingi .

Mwenyekiti wa bodi ya CFF Davis Malombe alaifiki uhuru wa vyombo vya habari nchini Kenya umepata maendeleo makubwa na changamoto kwa miaka mingi.

“Kama nguzo muhimu ya demokrasia vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuunda maoni ya umma, kuwawajibisha viongozi na kuwajulisha wananchi matukio mbali mbali,” alisema Malombe.

Mwenyekiti wa CFF Davis Malombe

Aidha alidokeza kuwa mazingira ya vyombo vya habari nchini Kenya yamekabiliwa na vikwazo vingi vikiwemo kuingiliwa kisiasa, vitisho kwa waandishi wa habari, vikwazo vya upatikanaji wa habari, kupungua kwa vyanzo vya mapato na kusababisha wasiwasi juu ya uendelevu wa vyombo vya habari,

Kwa upande wake mkurugenzi wa KCA William Oloo Janak alisema kuwa tangu mwaka 1992 vyombo vya habari na mashirika ya kijamii yamechochea mageuzi katika nchi hii yaliyopelekea kurejea kwa siasa ya vyama vingi,

“Mazungumzo ambayo tunajaribu kuyatilia mkazo kati ya vyombo vya habari na mashirika ya kijamii ni njia mojawapo ya kujenga nguvu ,kwa sababu mashirika ya kijamii yako na uwezo mkubwa wa uchunguzi, mipangilio ya kazi na motisha kwa waandishi wa habari. Hivyo ushirikiano wao utaweza kulinda nafasi ya kiraia,” alsema Janak.

Mkurugenzi wa KCA Oloo Janak

Janak aliongeza kuwa kongamano la kwanza la waandishi habari na mashirika ya kijamii liliangazia kwa kina mbinu mbalimbali za kutatua changamoto zilizozingira uhuru wa vyombo vya habari na mashirika ya kiraia, akisitiza umuhimu wa kuandaa kwa kongamano hilo kila mwaka ili kuweza kufuatilia kwa ukaribu endapo mbinu zilizopo zitazaa matunda katika maswala ya utetezi wa kiraia.

Afiss mkuu mtendaji wa baraza la vyombo vya habari nchini Kenya (MCK) David Omwoyo amethibitisha jumla ya kesi 79 za ukiukaji wa haki za waandishi habari zilirekodiwa wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024.

“Kati ya hizi kesi 79 nusu yake zimeripotiwa katika maeneo ya mashinani, tumeona baadhi ya watu mashinani wakitengeneza mazingira magumu ya kazi kwa waandishi habari,” alisema Omwoyo.

Omwoyo alitoa changamoto kwa mashirika ya kijamii na waandishi habari kujenga misingi bora ya  utendakazi ili kuhakikisha haki zao hazikiukwi.

Hata hivyo alisema kuwa kukosa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kwa washukiwa wa ukiukakaji wa haki za waandishi wa habari huchochea kuongezeka kwa dhulma dhidi ya wanahabari,

Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK David Omwoyo

“Kuna haja ya kutafuta mbinu za kuwachukulia hatua washukiwa wote wanaotishia maisha wanahabari, kushinda kuwafikisha katika mikono ya sheria kumepelekea hata familia za waandishi wa habari kupitia dhulma hizi,”aliongeza Omwoyo.

Wakati uo huo amewaonya vikali baadhi ya waandishi habari wanaohatarisha maisha ya wenzao kwa kutoa ripoti za habari zinazofuatiliwa kwa wahusika kuwa atakayepatikana atakabiliwa kisheria,

“Hili jambo limekuwa donda sugu baina ya waandishi habari, utapata mwandishi habari anachukua siri kwa kikundi chao cha Whatsapp na kusambaza kwa wahusika, hii ni hatari sana na hatutaivumilia kama baraza la vyombo vya habari,”Omeoyo alisema.

Scroll to Top