Hamisi Koja ahifadhi wadhfa wake wa FKF Kwale

Na Rasi Mangale

Hamisi Koja amehifadhi kiti chake cha mwenyekiti wa shirikisho la kandanda nchini (FKF) tawi la kaunti ya Kwale katika uchaguzi uliotamatika.

Koja alizoa kura 34 ya mpinzani wake wa karibu Mohammed Omar Nyonyo aliyepata kura 4.

Abdallah Makoro alichaguliwa katika nafasi ya katibu baada ya kupata kura 34 dhidi ya Jeoffrey Mumbo aliyepata kura 4 pekee huku Bakari Hamisi Zamu akishinda nafasi ya mwekahazina kwa kupata kura 31 dhidi ya Abdallah Dzengo aliyepata kura 7.

Kwenye uchaguzi huo wa kaunti ya Kwale ni wajumbe 38 waliokuwa wakipiga kura.

Katika kaunti ya Mombasa mambo yamemuendea sambe jambe Lillian Kazungu baada ya kupoteza nafasi ya mwenyekiti na nafasi hiyo kuchukuliwa na Alaamini Abdallah.

Lilian ambaye amekuwa katika nafasi ya mwenyekiti wa FKF kaunti hiyo kwa muda amebwagwa baada ya kupata kura 22 dhidi ya 26 za mpinzani wake.

Huko Kilifi kigogo wa soka na mwenyekiti FKF Dickson Angore ametetea kiti hicho baada ya kujizolea kura 34 na kumbwaga mpinzani wake Mohammed Kai aliyepata kura 24.

Nafasi ya katibu huko Kilifi ilimwendea Tom Onyango baada ya kumrambisha sakafu Japheth Kaingu kwa kura 39 dhidi ya 19.

Mohamed Salim alishinda nafasi ya mwekahazina akipata kura 41 na kumpiku Juma Makarani aliyepata kura 18.

Kwenye nafasi ya mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kilifi, Elizabeth Hinzano alimwangusha Maureen Munyazi kwa kuwa kura 42 dhidi ya 16.

Katika uwakilishi wa vijana kaunti ya Kilifi, James Kazungu amepata kura 35 na kumbwaga mpinzani wake Edward Nyinge aliyepata kura 24.

Uchaguzi wa urais wa FKF unatarajiwa kufanyika tarehe 7 Disemba mwaka huu baada ya ule wa kaunti kukamilika.

Scroll to Top