Na Caroline Katana
Shirika la utafiti wa kilimo na mifugo nchini KALRO linaendeleza zoezi la kukusanya sampuli za udongo katika kaunti 45 za humu nchini ili kutoa mapendekezo kwa serikali kuhusiana na swala la utumizi wa mbolea katika kila kaunti hizo, baada ya zoezi la utafiti katika maabara kukamilika .
Malengo ya utafiti huo ni kuhakikisha wakulima wanajua afya ya udongo wao na kutumia mbolea iliyo sahihi katika mashamba yao ili kuinua viwango vya uzalishaji na kupunguza gharama za ununuzi wa chakula kutoka mataifa ya nje.
Zoezi hilo lililotia nanga mwezi huu na kutarajiwa kukamilika mwezi Machi, linafadhiliwa na serikali ya Kenya na benki kuu ya dunia.
Taifa la Kenya kwa sasa likiwa limepunguza kwa asilimia 30 uagizaji mahindi kutoka mataifa ya nje tangu serikali kuanzisha mpango wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima.
Licha ya mpango huo wa mbolea ya bei nafuu kutekelezwa na serikali wakulima hawana habari sahihi za aina ya mbolea wanayofaa kutumia.
Mwanasayansi mkuu wa utafiti katika kitengo cha mazingira, udongo na mali asili katika shirika la KALRO Michael Okoti, aliyekuwa akizungumza na waandishi habari katika afisi za KALRO Matuga, kaunti ya Kwale amesema kuwa mkulima anafaa kujua hali ya udongo wa shamba lake kila baada ya miaka mitatu.
“Kisayansi mkulima anafaa kujua hali ya mchanga wa shamba lake baada ya kuutumia, kwa miaka mitatu, ambapo mkulima atalipa ada ya shilingi 900, baada ya zoezi hilo linalogharamiwa na serikali kukamilika,” alisema Okoti .
Aidha mwanasayansi huyo amesema kuwa kaunti ya Kwale iko na vituo 1,300 vya kuchukua sampuli za udongo ambavyo zimetengwa kwa njia za kiutaalam na vitawakilisha kaunti nzima ya Kwale wakati majibu yatakapotolewa .
“Utafiti wa mchanga Kwale utafanyika katika kila wadi na wakulima watajulishwa matokeo, ili wajue aina ya mbolea ya kutumia katika mashamba yao ili kuboresha mazao,” aliongeza Okoti
Kadhalka amedokeza kuwa KALRO kwa ushirikiano na wadau wengine wako mbioni kuunda mfumo wa kidijitali utakaowawezesha wakulima kujua mbolea hitajika kwa mashamba yao kabla ya mwaka huu kukamilika.
Msimamizi wa kituo cha KALRO Matuga Finyange Pole, amesema kuwa wakulima wengi hususan eneo la pwani wamekuwa wakilima bila kutumia pembejeo kama mbolea hatua inayowapelekea kupata mazao duni kila msimu wa mavuno.
“Wakulima wanapaswa kujua kuwa kila wakati wakilima na kuvuna wanapunguza rotuba kwenye mchanga, hivyo wakati umefika sasa wametumie mbolea iliyo sahihi kwa mimea yao,” alisema Pole .
Wakati uo huo amewataka wakulima kukomesha mila na itikadi potofu dhidi ya utumizi wa mbolea.

Msimamizi wa kituo cha KALRO Matuga, Dkt Finyange Pole
“Hapa Kwale kuna wakulima hata ukiwapatia mbolea bila malipo hawataitumia, wako na dhana potofu kuwa mbolea inaharibu mchanga, jambo ambalo sio la kweli,” aliongeza Pole.
Ametoa changamoto kwa wakulima eneo la Kinango na wadi ya Dzombo huko Lungalunga kukomesha itikadi hizo kwa manufaa yao.
“Wakati mwingine hata tukienda kuchukua sampuli za mchanga wengine hata hutufukuza wakidhania kuwa tunaenda kuuza mchanga ama kuupeleka kwa washirikina ili kuwaharibia mazao yao, na sisi malengo yetu ni kuhakikisha wanatumia mbolea iliyo sahihi na kuongeza mazao yao,” Pole alisema.
Wakati uo huo ameeleza kuwa licha ya eneo la Pwani kuwa na uwezo wakujilisha na kulisha kaunti zengine, bado eneo hilo linauzalishaji wa chakula wa asilimia 30 pekee, likisalia kutegemea chakula kutoka kaunti zengine za humu nchini.
“Sekta ya kilimo ili gatuliwa na ni jukumu la kila kaunti walipe kipaombele swala za uzalishaji wa chakula ,na tukilisha watu wetu vizuri hakutakuwa na haja ya kujenga hospitali na zahanati nyingi mana magonjwa mengi haswa yale yasiyoambukiwa yanakuja kwa kukosa lishe bora,” alisisitiza Pole .
Beauty Tatu Matata kutoka kijiji cha Tumbula wadi ya Waa –ng’ombeni ni mkulima na mfugaji anayeendeleza kilimo biashara ambaye amehiari kufanyiwa upimaji wa udongo wa shamba lake.
“Ningependa sana kupimiwa huu mchanga ili niweze kujua aina ya mbolea ninayofaa kutumia ili niweze kupata mazao mengi Zaidi yatakayo nipa faida kubwa,”alisema Tatu.
Aidha ameeleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi, uvamizi wa wadudu na wanyamapori ni baadhi ya changamoto sugu zinazolemaza kilimo chake.

Beauty Tatu Matata, mkulima, kijiji cha Tumbula, wadi ya Waa/Ng’ombeni
“Ukilima mahindi inakulazimu ueke ulinzi hadi siku ya kuvuna ,huku kuna uvamizi wa nguruwe, ndege na nyani ila kuutaja uvamizi wa wadudu kwenye mimea kumnyima lepe la usingizi,” aliongeza Tatu.
Tatu akisema kuwa ndoto yake ni kuwa mkulima wa kimataifa, akiitaka serikali ya Kwale na wadau mbali mbali wa kilimo kujitokeza na kusaidia wakulima kukabiliana na changamoto hizo.
“Nilipenda kilimo tangu nikiwa mtoto mdogo na ningependa kudumu katika kilimo ,maono yangu ni kuzalisha chakula Zaidi cha matumizi ya nyumbani na kibiashara ,maana hii ni ajira binafsi,” aliongeza Tatu.
Ali Omar Siri ni mkulima na mfugaji katika eneo la Patanani ambae pia amelipokea vyema zoezi la upimaji wa udongo unaoendelezwa na shirika la KALRO.

Ali Omar Siri, mkulima, kijiji cha Patanani
“Zoezi hili ni muhimu sana, kwa maana utajua mapungufu yaliyopo katika mchanga na itakuwa rahisi kujua aina ya mbolea sahihi yakutumia ili niweze kupata mazao bora Zaidi , mchanga huu uko na madini tofauti tofauti kwa hio baada ya utafiti nitajulishwa ni kipi cha kufanya ili uzalishaji uboreke,” alisema Siri .
Siri amewataka wakulima kaunti ya Kwale kukumbatia zoezi hilo linalolenga kuboresha mazao na kuhakikisha usalama wa chakula katika siku za usoni, kwani kwa miongo mingi kaunti ya Kwale imekuwa ikikumbwa na makali ya njaa.












