Na Kwale Press Club
Gavana wa kaunti ya kwale Fatuma Achani amepiga marufuku mikutano inayofanywa baina ya na baadhi ya wanasiasa na makundi ya vijana wadogo wenye kutumia mapanga katika eneo la Diani huko Msambweni.
Achani amesesema mikutano hiyo inalenga kuchochea vijana kuvuruga amani Katika eneo la Diani.
Akizungumza huko Diani wakati wa uzinduzi wa taa za barabarani za kutumia miale ya jua, gavana huyo amesema kuwa vijana wanaojihusisha na uhalifu ni watoto wadogo chini ya miaka 17 wasiopaswa kuajiriwa.
Amevitaka vitengo vya usalama kukabili wanasiasa wanaotumia vijana wa panga kwa malengo yao ya kisiasa’
Aidha ameagiza idara ya usalama kuwakamata wanasiasa wanaofanya mikutano na vijana wahalifu.
“Na wale viongozi ambao wanakaa na kuchochea vijana ili vijana wawashambulie wananchi naomba wakome tabia hiyo. Hakuna mtu amabaye ako na haki atoke na vipanga ati kwa kusemekana hana ajira ili akapige mwingine panga, hiyo tunasema tumekataa na wanaofanya mikutano hiyo haramu tunawaangalia na tunawapatia notisi” alisema Achani.
Gavana aliongoza kuwa “Hii kaunti hatutakubali eti vijana wadogo wa miaka 17 eti hawana ajira wanaenda kupiga watu mapanga. Kijana wa miaka 17 ni motto huyo atapatiwa kazi gani?”
Achani vile vile akiwataka wazazi kujukumika na watoto wao na kusema kuwa serikali yake inaendelea na mradi wa basari ili kuona kuwa mtoto wa kwale anafadhiliwa masomo yake katika shule za secondary, vyuo vikuu na vya anwai na kuwataka vijana kusitisha visa vya kihalifu na kujitosa katika ujenzi wa taifa.
“Hao ni watoto washike basari waende wasome tusiseme eti vijana wadogo wameshika mapanga mtu ameamka anasema ameenda kutafuta riziki yangu sokoni wampiga panga alafu mnataka tuwatetee?” alisema Achani.
Achani amesema serikali ya kaunti pia itawapa ajira vijana walio na rekodi nzuri.
“Wale wengine ambao ujuzi wako nao na kama rekodi yako ni safi utapatiwa kazi ya kufanya. Ata huyu mkandarasi ambaye leo tumempatia tenda hii atapena kazi laki hawezi patia mtu mhalifu kazi” aliongeza Gavana.














