Na Caroline Katana
Waziri wa madini na uchumi wa bahari na majini Ali Hassan Joho amewataka baadhi ya watu waliowasilisha kesi mahakamani kupinga kamati ya kupangalia utumizi wa ardhi ya Base Titanium baada ya uchimbaji madini kuiondoa ili kutoa nafasi ya mazungumzo.
Watu hao wanadaiwa kuwasilisha kesi ya kutafuta haki ya umiliki wa ardhi iliyoachwa na kampuni hiyo baada ya kukamilisha muda wake mwaka uliopita.
Waziri Joho alisema kuwa mazungumzo kati ya serikali na wakaazi ndio njia pekee ya kupata mwafaka wa jinsi ardhi hio itakavyotumika na wala sio kuenda mahakamani.
“Sisi hapa ni watu wa moja, ni ndugu moja, ni mwana wa mjomba na wa shangazi shauku nataka tuzitoe, kile kitu cha kufanya ni sisi kwa sisi tuzungumze, hakuna mtu mwengine atatufanyia maamuzi, twafanya uamuzi wenyewe. Zzamani sisi tulikuwa na mila nzuri ukiteleza waitiwa wazee si turudie hizo mila, tuite wazee ili mambo yasonge mbele. Wale ndugu zetu walioenda kortini tutafanya nao kazi kwa ukaribu waondoe hio kesi ,” alisema waziri Joho .
Katika ziara yake ya awali ya kutathmini zoezi la urekebishaji sehemu zilizochimbwa madini waziri Joho alishikilia kuwa ardhi iliyotumika na kampuni ya Base Titanium itasalia katika himaya ya serikali kuu.
Akisema kuwa ardhi hio iko ina uwezo wa kufanyiwa miradi mikubwa ya kilimo na kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji ili wajiendeleze kiuchumi badala ya kurudishiwa wenyeji ambao huenda wakaingiwa na tamaa ya kuiuza.
Joho alionya viongozi na wakaazi dhidi ya kuchochea swala hilo kisiasa.

Shemu iliochimbwa madini na Base Titanium
“Vijana 1,600 wanaokosa ajira baada ya kampuni ya Base Titanium kuondoka wanahitaji mwafaka kutoka kwa viongozi hivyo ni sharti mipangilio iafikiwe kwa wakati ili waweze kufaidika na miradi itakayotekelezwa katika ardhi hio, ningeomba mbunge wa msambweni Feisal Bader na viongozi wengine wafuatilie hili jambo la kuondoa kesi kortini ili tusonge mbele,” alisema waziri Joho.
Wakati uohuo ametoa amri ya kufutiliwa mbali kwa leseni za uchimbaji madini zilizopeanwa kwa waekezaji zaidi ya miezi 6 iliyopita ambao hadi kufikia sasa bado kuanza shughuli za uchimbaji .
“Kama mtu amepewa nafasi ya uchimbaji madini na haitumii aende akienda tu asitusumbue, tutafute mtu ambae atafanya shughuli hio kikamilifu nataka katibu wangu aanzishe huo mchakato wakuzifutilia mbali hizo leseni,” alisema.
Alisema kuwa swala la madini ndio mwanzo linatekelezwa kwa njia ya kueleweka humu nchini hivyo ni sharti swala hilo lizingatie haki.
“Katika mazungumzo ya madini kuna kitengo cha jamii, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa , ni haki jamii ipate fungu lake na serikali pia,”aliongeza .
Waziri huyo pia ametoa agizo kwa kamishna wa kaunti ya Kwale Stephen Orinde na gavana wa Kwale Fatuma Achani kusimamisha uchimbaji haramu wa madini unaotekelezwa kaunti ya Kwale.
“Msiningoje mimi nije huku ndio nitoe agizo la kusimamisha uchimbaji haramu wa madini, hii ni mali ya umma, kama mtu hajatambua jamii pambaneni nae ,msiningoje mimi nitoe agizo hilo,” alionya Joho .
Hata hivyo ameitaka jamii kuhakikisha wanaekeana mkataba wa maelewano na wachimbaji madini wadogo wadogo kama wale wanaochimba mchanga wa kutengeza vioo ili kuepuka dhulma.
“Ni vyema jamii kujua tathmini ya madini yao kisha waandikishiane mkataba na waekezaji kwa mipango maalum kama vile kampuni ya uchimbaji ya basetitanium ilivyokuwa ikifanya, kujenga mashule ,zahanati ,kulipa asilimia moja ya faida ya madini na saa hii basetitanium imelipa ruzuku kwa serikali, iliyobaki ni mimi kuchukua hio asilimia 20 ya serikali ya kaunti ya Kwale na ile asilimia 10 ya wakaazi, Kwale ndio kitovu cha uchimbaji madini na ni sharti tuwafundisheni wengine ,msikubali kupoteza sifa za uchimbaji mlizojenga,” alisema.
Usimamizi wa Base Titanium ulisafirisha shehena ya mwisho ya madini mnamo tarehe 12 mwezi February 2025 ikiwa shehena ya 171 tangu mwaka 2014, serikali ya kitaifa ikisalia kutoa ahadi ya kutoa mirahaba kwa wakaazi hata licha ya aliyekuwa waziri wa madini Salim Mvurya na waziri wa sasa wa madini Ali Hassan Joho kukiri kwamba usimamizi wa Base Titanium hauna deni na serikali ya Kenya.












