Kwale yaziba pengo la wahudumu wa afya walioathirika na kusitishwa kwa ufadhili na Marekani

Na Caroline Katana 

Kaunti ya Kwale imelazimika kuekeza zaidi katika wizara ya afya katika mwaka huu wakifedha wa 2025/2026 ili kupata nafasi ya kuajiri wahudumu wa afya zaidi ili kujaza pengo lililoachwa na wahudumu wa afya waliokuwa katika mpango wa ufadhili wa USAID kupitia shirika la USAID Stawisha Pwani .

Tangazo la tarehe 24 Januari la kusitisha  mabilioni ya Dola za ufadhili wa marekani kwa programu zote za misaada ya kigeni  kwa muda wa siku 90  lililazimu takriban wahudumu wa afya  50 waliohudumu katika mpango huo kusitisha shughuli zao kaunti ya Kwale.

Wahudumu hao wa afya walikuwa wakitoa huduma katika kitengo cha HIV/AIDS, kifua kikuu, Malaria na ushauri katika vituo mbalimbali vya afya kaunti ya Kwale.

“Watu walikuwa wameajiriwa ili waweze kutoa huduma lakini kwa sasa hawako tena katika hospitali zetu, wahudumu hawa walikuwa wametuongezea ile idadi ya wahudumu wa kaunti kwa sababu tulikuwa na  washauri, wauguzi  na madaktari wa kutosha, lakini sasa inabidi kama kaunti tujipange ili kuhakikisha utoaji wa huduma hausimami,” alisema waziri wa afya kaunti ya Kwale francis Gwama.

Serikali ya Marekani ilifadhili takriban asilimia 47 ya misaada ya kibinadamu duniani mwaka jana.

Kabla ya kuapishwa mwezi Januari Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametia saini amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa shirika la afya duniani  (WHO) na hii ikiwa ni mara ya pili kwa Trump kuamuru Marekani kujiondoa kuwa mwanachama wa WHO  .

Trump alikosoa jinsi shirika hilo la kimataifa lilivyoshughulikia janga la Covid -19 na kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka kwa taasisi hiyo ya Geneva wakati wa janga hilo.

Gwama amesema kuwa huduma hizo maalum za afya zinaendelea kutolewa japo sio kama ilivyokuwa awali.

“Tumewashauri wahudumu wetu wa afya katika zahanati na vituo vya afya waweze kutoa huduma zote, mipangilio imebadilika sio kama awali ambapo kila muhudumu wa afya alikuwa akishughulikia kitengo chake, kufuatia pengo lililopo sasa muhudu katika zahati atalazimika kuwahudumia wagonjwa wote kwa usawa ili kuhakikisha afya endelevu,” alisema Gwama .

Mshirikishi wa maaambukizi ya virusi vya HIV/ na maradhi ya zinaa Nana Mafimbo amethibitisha watu 15,000 wanaishi na virusi huvyo kaunti ya Kwale.

“Wengi wa watu wanaoishi na virusi vya HIV ni wanawake ila takwim zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yameathiri sana vijana na watu wa hadi umri wa miaka 24,” alisema Nana.

Licha ya wanaume kuwa na idadi ya chini ya maambukizi ya virusi vya ukimwi bado idadi ya vifo miongoni mwao iko juu ikilinganishwa na ile ya wanawake.

“Vifo vya wanaume viko juu kwa sababu hawajajikubali na hata wakiwa kwa mpango wa matibabu hawafuatilii kanuni za utumizi wa madawa za kupunguza makali ya virisi vya HIV (ARVs), na baadhi ya wanaume ambao hawajikubali hufanya mapenzi bila kinga ‘wakisema sitaki kufa peke yangu’ hatua ambayo inawafanya kupata maambukizi mapya yanayowaeka katika hatari zaidi huku baadhi ya wanaume hao wakijitosa katika maswala ya ulevi,”alisema waziri Gwama.

Hata hivyo mshirikishi huyo amesema kuwa kwa sasa madawa hayo yaliyofadhiliwa na shirika la USAID yataendelea kupatikana kaunti ya Kwale kwa muda wa miezi 7.

“Kwa sasa tuko na madawa ya kututosha ya miezi mitatu katika vituo vyetu vya afya na katika serikali ya kitaifa KEMSA wako na dawa zakutosheleza miezi mine, hivyo kwa muda wa miezi 6 au 7 wagonjwa watapata dawa,” alisema Nana.

Nana aliongeza kuwa endapo Marekani haitolegeza kamba katika msimamo wake serikali ya kitaifa na zile za kaunti zitalazimika kutafuta mwafaka wa pamoja ili kuhakikisha wagonjwa wanaendelea na tiba zao.

“Huduma za afya ziligatuliwa lakini bado serikali ya kitaifa iko na majukumu makuu hususan katika maswala ya viwango na ubora wa dawa  inasalia katika himaya ya serikali kuu,” alisema Nana.

Scroll to Top