Kenya Power yaboresha huduma na kuwaonya wezi wa umeme Kwale

Na Caroline Katana   

Usimamizi wa kampuni ya usambazji umeme nchini Kenya Power tawi la Kwale umewaonya baadhi ya watu wanaojihusisha uunganishaji wa stima kinyume cha sheria na wizi wa vifaa vinavyotumika kuunganisha stima kuwa atakayepatikana atakabiliwa kisheria.

Wizi wa mita, transfoma, conductors na nyaya umesemekana kusababishia kampuni hiyo kukadiria hasara kubwa na kuhujumu utendakazi wake.

“Tumekuja kufahamu kuwa huu uunganishaji umeme usiokuwa halali hutekelezwa kwa kutumia vifaa vyetu vinavyoibwa katika vituo vyetu vingine. Tukipata wizi kama huo sisi hutenganisha hizo nyaya nakuziunganisha upya. Tabia hii tunataka ikome mara moja. Tunaambia wateja wetu wanaojipata katika hatia hio wafike katika afisi zetu na wafanye taratibu za kisheria za uunganishaji stima,” alisema meneja wa Kenya Power Kwale Erick Momanyi.

Kampuni hio ikiwa na wateja takriban elfu 90 katika kaunti ya Kwale. Idadi inayotarajiwa kuongezeka hata zaidi kufuatia uhitaji mkubwa wa nguvu za umeme miongoni mwa wakaazi. .

Momanyi amesema kuwa kampuni hio iko na vituo vidogo vinne vya kusambaza nguvu za umeme huku hujudi za kuongeza vituo zaidi zikiafikiwa ili kutatua changamoto ya ukosefu wa nguvu za umeme unaoshuhudiwa na wateja wao mara kwa mara.

Meneja wa Kampuni ya Kenya Power, Kwale, Erick Momanyi

“Kuna kituo cha usambazaji nguvu za umeme kinajengwa pembezoni mwa mji wa Kwale. Kituo hiki kitasambaza umeme eneo la Kinango na Kwale mjini na viunga vyake. Tunajua kuwa zile nyaya zinazosambaza umeme Kwale na Kinango ni ndefu sana, kwa hio uwepo kwa kituo hicho kitafupisha na kuongeza nguvu zaidi za umeme na kuhakikisha wakaazi wanapata huduma bora,” alisema.Momanyi.

Kadhalka amewataka wakaazi kuchukua tahadhari dhidi ya walaghai wanaojifanya kuwa maafisa wa Kenya Power na kuwapora fedha zao.

“Mtu anayekuitisha pesa ndio akuekee stima huyo ni mtu unafaa kumripoti katika afisi zetu kwa sababu usimamizi wa kampuni hii hutoa nukuu ya mwongozo wa malipo. Mtu akitaka kuunganishiwa stima afike katika afisi zetu asilaghaiwe,” aliongeza.

Hata hivyo amewaonya wakaazi dhidi ya kutumia nguzo za stima kama kuni kuwa hatua hio inahatarisha afya zao.

“Hizi nguzo hazijaidhinishwa kutumika kama kuni kwa sababu ziliekewa dawa ya kuua mchwa kwa hio zikichomwa hutoa hewa yenye sumu ambayo madhara yake huonekana baadae, kwa hio kwa usalama wa afya zao wasichome hizo nguzo, hata wakiona hizi nguzo zimekaa chini kwa muda mrefu inamaana kuna mradi unataka kuanza kwa sababu kila mradi wa kuunganisha stima huwa na utaratibu wake kwa hio wakaazi wawe na subra badala ya kuzipasua kuni,”alisema Momanyi

Akigusia swala la uchomaji wa nguzo za umeme maneja huyo amewataka wakaazi kukomesha tabia za kutayarisha mashamba yao kwa kutumia moto, akiitaja hatua hio kuathiri pakubwa huduma za usambaji stima pamoja na kusababishia kampuni hasara.

“Msimu huu watu wamekuwa wakichoma mashamba ambapo nguzo za stima pia zimekuwa zikichomeka, na hii imekuwa changamoto kubwa kwani imekuwa ikisababisha kukatika kwa nguvu za umeme,”alisema.

Msimamizi wa kitengo cha wateja wa Kenya Power, Kwale, Kelly Joy Kithinji

Msimamizi wa kitengo cha kusimamia wateja katika kampuni hio tawi la Kwale Kelly Joy Kithinji alisema kuwa kwa sasa wameanzisha mpango wakueka mita za kisasa almaarufu smart metre kwa wateja wao kama njia moja ya kukabiliana visa vya wizi.

“Tumekuwa na mita za moto tofauti tofauti, tulianza na zile za kitambo ambapo afisaa wetu angelazimika kuzunguka kusoma hio mita, tukatoka huko tukaenda kwa token ambayo ni lazima ununue stima kabla kutumia, hivi sasa tumeanzisha mita nyengine inaitwa Smart Metre, hii mita sio lazima mtu aje kuisoma, hii inajisoma yenyewe, ikikutolea bili yako inafaa ulipe kwa wakati ama inajizima hadi ulipe bili yako na pia utalipa faini ya shilingi 580 kwa kuchelewa ndiposa  upate stima upya, Hii mita imetusaidia sana kwa sababu inapunguza wizi wa umeme kwa maana mtu akiigusa tu inajizima, kwa hio ina manufaa makubwa kwa kampuni, ningeomba maafisa wetu wakija muwakubalie waeke mita hii,” alisema Kithinji. .

Kithinji akisema kuwa anaendeleza misururu ya hamasa mashinani kuhusiana na maswala mbalimbali ambayo wakaazi wanapaswa kuyafahamu katika swala zima la utumizi na ulinzi wa stima kwa usalama wao.

“Awali tulikuwa tukirekebisha tatizo la stima  tulikuwa hatuelezi wakaazi lakini kwa sasa tumelichukua kama jukumu letu, kama tunataka kuondoa matawi ambayo yameshikana na nyaya za stima tunawaeleza mapema pamoja na vifaa vitakavyotumika, pia tunawaelimisha wananchi athari za uchomaji nguzo za stima wakati wanapotayarisha mashamba yao, tunawaelezea pia taratibu wanazofaa kufuata ili wapate umeme kwa njia halali na salama, miongoni mwa maswala mengine muhimu ya kampuni yanayowahusu,” aliongeza.Kithinji.

Akigusia swala la usalama Kithinji amesema kuwa ni sharti wateja wao wawe wangaalifu wanapotumia stima.

“Stima ni nzuri kwa kila mtu lakini ina hatari yake, tunawatahadharisha wateja wetu kuwa  ni hatari kufunga kamba za kuanika nguo chini ya mabati ya nyumba kwa sababu nyaya za umeme zikilegea na kuangukia kamba hizo za nguo zikiwa na maji inakuwa hatari kwa usalama wao ni vyema kamba za nguo zifungwe nje ya nyumba,”alisema.

Kithinji aidha amewataka wateja wao kutumia nambari ya *977# ama wapige simu kwa 9771 ili wapate huduma za Kenya power moja kwa moja.

“Kupitia nambari hizi wakaazi wataweza kuripoti  kisa chochote na pia wataweza kubaini maafisa halali wa Kenya Power na walaghai kwa sababu kuna chaguo ya Jua For Sure ile ambayo unajua ni nani haswa anayekuhudumia ,ukimuomba nambari yake ya kitambulisho na ile ya kazi itakueleza kama yeye ni mfanyikazi  wa Kenya Power ama ni mlaghai,” alisema.Kithinji.

Usimamizi wa Kenya Power Kwale sasa umewataka wateja wao kutarajia huduma bora zaidi za usambazaji umeme hata wakati wa msimu wa mvua baada ya kufanya ukarabati wa mitambo na nguzo zilizokuwa katika hatari ya kuanguka.

Scroll to Top