Na Bintihamisi Kadide
Wakaazi wa visiwa vya Wasini n Mkwiro huko Shimoni eneo bunge la Lungalunga kaunti ya Kwale wanaitaka serikali ya kaunti hiyo kupitia wizara ya afya kuwapelekea ambulensi za boti.
Wanasema ambulensi hizo zitasaidia kupunguza visa vya akina mama kupoteza maisha kunapotokea dharura inayohitaji kuvuka kufika Shimoni mjini.
Wakaazi hao walalamikia kutengwa katika baadhi ya huduma mbali mbali ambazo zingewafaidi kama wakaazi wa kaunti hiyo.
Wakiongozwa na Khadija Mohamed kutoka kisiwa cha Mkwiro wamesema kuwa akina mama wengi waja wazito wamekua wakipoteza maisha na wengine kujifungua katikati ya bahari na wakati mwengine bandarini wakisubiri kuabiri dau.
Khadija amesema kuwa kutokana na ukosefu wa huduma za afya nyakati za usiku inawalazimu kupitia changamoto hizo huko isiwani.
Fariya Juma kutoka kisiwa cha Wasini amesema kuwa kukosekana kwa mhudumu wa kuwadumia kila mara katika visiwa hivyo ni kero na tishio kwa maisha yao.
Anasisitiza kuwa baadhi ya watu wamepoteza maisha kutokana na umbali wa kituo cha afya kilicho na huduma zote za afya ambazo zinatolewa wakati wowote.
Wanaitaka serikali ya kaunti ya Kwale kuwawekea mhudumu wa usiku sawia na wadi itakayowasaidia kupata huduma za afya kila wakati.












