Na Caroline Katana
Ni ushahidi gani unahitajika Kuonyesha uwezo wa wanawake katika uongozi? Kuna dhana ambayo bado imo kwa baadhi ya watu kuwa wanawake hawana uwezo wa kumudu majukumu ya uongozi.
Dhana hii imepata nafasi katika jamii kutokana na historia ya jinsi zilivyokuwa zikimchukulia mwanamke kwa muda mrefu.
Jamii nyingi duniani zimemchukulia mwanamke kama kiumbe dhaifu, asiyekuwa na uwezo wa kufanya yale ambayo wengi wamezoea kuona yakifanywa na wanaume na kwamba mahala pake ni jikoni au chumbani “akimpumbaza “ mumewe baada ya kazi na kulea watoto.
Kinachomtofautisha mwanamume na mwanamke ni vitu vichache sana kama wataalamu wanavyosema asichoweza kukifanya mwanamke ni kitu kimoja tu kwamba “ hawezi kupeana ujauzito” tu basi, lakini taja vyenginevyo vyote utakavyotaja anaweza na mwanamume nae mbali na bidii zake zote hawezi “kubeba mimba na kunyonyesha .
Fatuma Chaunga ni miongoni mwa wanawake katika jopo la bajeti kaunti ya Kwale linaloongoza vikao vya umma vya kutathimini miradi iliyoorodheshwa katika makadirio ya bajeti ya Billion 9.7 ya mwaka wakifedha 2025/26 vilivyong’oa nanga Aprili 22 2025.

Fatuma Chaunga, mwanajopo wa jopo la Bajeti kaunti ya Kwaleaa
“Wakaazi wako na fursa ya kuitambua miradi waliyoipendekeza wakati wa vikao vya kutoa maoni ya kupendekeza miradi ,na endapo watapata mabadiliko ya aina yoyote, wanahaki ya kutoa mapendekezo ya marekebisho, na tunanukuu kila maoni ya wakaazi na tutayawasilisha kwa wahusika ili kuona kuwa matakwa yao yanatekelezwa kwa haki na usawa, vikao hivi vitakamilika siku ya Jumamosi 25 “ alisem Chaunga.
Kwenye mahojiano kwa vyombo vya habari pembezoni mwa vikao hivyo katika ukumbi wa Kombani na Ramisi, Chaunga ametoa changamoto kwa wanawake kujitokeza ili kujengwa uwezo, wapate fursa ya kujikuza kiuchumi, maendeleo na uongozi.
“Jinsi tunavyoona wanaume wakijitokeza wakitaka kujijenga nisharti wanawake pia wakubali kubadilika na kujijenga kwani fursa ipo,” aliongeza Chaunga.
Chaunga amewataka wanawake kukomesha tofauti ndogo ndogo zilizowazingira na badala yake kuungana kwa minajili ya kujiendeleza.
“Haina faida kusimama katika majukwaa na kushambuliana kwa matusi, kuna haja ya wanawake kutia nia za kujikuza katika nyanja tofauti tofauti,” Chaunga alisema.

Kikao cha kutathmini miradi ya wodi ya Waa/Ng’ombeni katika ukumbi wa Kombani
Alisema kuwa wapwani wako na kila sababu za kujivunia kutokana na mifano bora ya viongozi wakike katika kanda hii.
“Sisi watu wa Kwale tunafaa tujivunie kwa kumpata mwanamke wa kwanza wakiislam kutoka kabila la wadigo kuongoza kaunti hii ya Kwale,” alisema Chaunga.
Hata hivyo amewataka wakaazi wa Kwale kuuheshimu utawala wa Kwale uliopo badala ya kuukejeli kwa maneno makali katika majukwaa.
“Ningependa kupeana mfano mzuri wa mbunge wa Likoni Mishi Mboko, amekuwa kwa uongozi kwa Zaidi ya miaka kumi na tano na sijasikia wanawake wakisimama kwa majukwaa na kumdhalilisha ,amepewa heshima kama kiongozi wakike ,hivyo nawaomba wakaazi wa Kwale kuiga mfano huo na tumheshimu gavana wetu wa Fatuma Achani,” alisisitiza Chaunga.
Kadhalka ameeleza kuwa serikali ya Kwale imekuwa ikiwezesha wanawake katika maswala ya uekezaji kupitia VSLA, umiliki wa kampuni, kilimo miongoni mwa maswala mengineyo ili waweze kuboresha maisha yao kinyume na ilivyokuwa hapo awali.
Akigusia swala la utekelezaji wa miradi bi.Chaunga ameitaka wizara husika na wawakilishi wadi kuhakikisha mapendekezo ya wakaazi kuhusu miradi yanapewa kipaombele ili kuhakikisha usawa wa maendeleo katika kila wadi za kaunti hio
Kifungu cha katiba (1) kinaeleza kwamba kila mtu ni sawa mbele ya sheria na ana haki ya kulindwa na kunufaika sawa : ibara ya 27 (3) inaeleza kuwa wanawake na wanaume wana haki ya kutendewa sawa ikijumisha haki ya fursa sawa katika Nyanja za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.












