Na Cece Siago
Waziri wa Madini, Uchumi wa Bahari na Masuala ya Baharini, Hassan Joho, amesema kuwa Kongamano la Our Ocean litakaloanza wiki hii mjini Mombasa linaipa Afrika fursa ya kipekee ya kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kimataifa kuhusu uhifadhi wa bahari na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Akizungumza mjini Mombasa kabla ya kuanza kwa kongamano hilo, Joho alisema mkutano huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utatoa nafasi ya kutathmini kwa kina namna rasilimali za bahari zinavyoweza kulindwa huku zikiendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Kongamano hilo linatarajiwa kuanza Jumanne, Juni 16, na kuhitimishwa Alhamisi, Juni 18.

Samaki wabichi wakikaushwa kwa jua huko Vanga, Kaunti ya Kwale. Uvuvi endelevu utakuwa miongoni mwa mada kuu zitakazojadiliwa katika mkutano huo. Picha na CeCe Siago
“Kongamano hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linatupa nafasi ya kujadili na kutathmini kwa kina masuala ya uchumi wa buluu. Kipaumbele ni kuangalia namna ya kulinda mazingira na kuhifadhi rasilimali hizi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” alisema Joho.
Aliongeza kuwa uwepo wa viongozi, wataalamu na wadau kutoka mataifa mbalimbali utawapa Wakenya fursa ya kujifunza jinsi nchi nyingine zilivyofanikiwa kuimarisha uchumi wa bahari kupitia sera na mikakati mbalimbali.
“Mazungumzo ya kimataifa yanamaanisha kuwa watu wetu watapata nafasi ya kuelewa sheria na mikakati iliyotumiwa na mataifa mengine kufungua fursa zilizopo. Muhimu zaidi ni kujifunza jinsi walivyoweza kulinda rasilimali hizi kwa manufaa ya sasa na ya baadaye,” alisema.

Waziri wa Madini, Uchumi wa Bahari na Masuala ya Baharini, Hassan Joho
Kongamano la Our Ocean linafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na linatarajiwa kuwaleta zaidi ya washiriki 6,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani kujadili masuala ya uhifadhi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, uvuvi endelevu na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Wakati huo huo, wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira katika ukanda wa Pwani wanataka jamii za wenyeji kupewa kipaumbele katika maamuzi na miradi itakayotekelezwa kutokana na kongamano hilo.
Wamesisitiza kuwa makubaliano na ahadi zitakazofikiwa hazipaswi kubaki kwenye karatasi pekee, bali zitekelezwe kwa vitendo ili kuleta matokeo yanayoonekana kwa jamii zinazotegemea bahari kwa maisha na riziki zao.
Mkurugenzi wa Samba Sports Youth Trust, Mohammed Mwachausa, ambaye huandaa shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira ikiwemo usafishaji wa fukwe, alisema mara nyingi jamii huwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira lakini hupata usaidizi mdogo wa kifedha.
“Fedha nyingi hutumika katika mikutano, lakini ni sehemu ndogo sana inayowafikia wanajamii na vijana wanaotekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira mashinani. Tungependa angalau asilimia 50 ya fedha za uhifadhi zielekezwe kwa jamii zilizo mstari wa mbele kutekeleza miradi hiyo,” alisema Mwachausa.
Kwa upande wake, afisa wa shirika la HERI Kenya linalojihusisha na masuala ya afya na mazingira katika Kaunti ya Kwale alisema ni muhimu mijadala ya kongamano hilo itafsiriwe kuwa hatua za vitendo zitakazowanufaisha wananchi wa kawaida.
“Suluhu nyingi hujadiliwa katika ngazi za juu bila kufikishwa kwa wananchi mashinani. Tunahitaji mapendekezo na suluhu zitakazopatikana kutafsiriwa na kusambazwa kwa jamii ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” alisema.

Afisa wa Shirika la HERI Kenya, Juma Nasoro
Naye Mkurugenzi wa Kwale Recycling Centre, Dexter Agesa, alisisitiza umuhimu wa kuongeza ufadhili kwa vikundi vya kijamii vinavyoendesha miradi ya uhifadhi wa mazingira.
“Jamii tayari iko mstari wa mbele kupitia miradi mbalimbali ya kulinda mazingira na inafanya kazi nzuri. Hata hivyo, miradi hiyo ingeweza kuleta matokeo makubwa zaidi iwapo kungekuwa na ufadhili wa kutosha,” alisema Agesa.
Wanaharakati hao wameeleza matumaini yao kuwa Kongamano la Our Ocean litakuwa tofauti na mikutano mingine ya kimataifa kwa kuhakikisha kuwa ahadi na makubaliano yatakayofikiwa yanaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii za pwani zinazotegemea bahari kwa maisha na uchumi wao.
Makala haya ni sehemu ya Ushirika wa Uandishi wa Habari wa Our Ocean 2026, ulioandaliwa na Internews Earth Journalism Network.












